Chama aishtukia Yanga mapema



Simba imecheza mechi 12 tu mpaka sasa kulinganisha na 15 ya vinara Azam na 14 za watani zao, ambapo alama zao 27 zimewafanya waachwe kwa tofauti ya pointi 11 na vijana wa Jangwani na 12 dhidi ya matajiri wa Chamazi
KIUNGO wa Simba, Cletous Chama ameiangalia kasi ya kikosi cha Yanga kisha akatoa neno juu ya matokeo yao, huku akichora ramani nzima jinsi Simba itakavyorudi kwa kasi na kuchukua taji lao mwisho wa msimu huu.
Yanga iliyopo nafasi ya pili ikiwa na alama 38, moja pungufu na walizonazo vinara, Azam iliyoifumua Mbao FC, inashuka Uwanja wa Taifa usiku wa leo kuvaana na Biashara, huku Simba iliyopo nafasi ya tatu ikiendelea kula shushu katika ligi hiyo.
Simba inajiandaa kwa mechi kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kucheza dhidi ya Nkana ya Zambia katika michezo ya raundi ya kwanza, ikianzia ugenini.
Chama alisema Yanga sio timu mbovu na kwa sasa wanafanya vema kuliko wao, ila Wekundu hao hawajakubali matokeo kirahisi.
Kiungo huyo anayeichezea pia Chipolopolo alisema kwa sasa Simba inatafuta uwiano mzuri wa kucheza kwa mafanikio mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu Bara na kwamba wakitulia Yanga wala pumzi yao haiwatishi.
"Yanga wanafanya vizuri sasa kuliko sisi, tupo nafasi ya tatu lakini haina maana kwamba Simba tumeridhika na hili tutarudi katika ligi hiyo kwa nguvu," alisema Chama na kuongeza; "Simba inapocheza mechi timu nyingine zinatukamia sana, ila zikicheza na Yanga zinafungwa kirahisi sana mpaka unashangaa najua hilo linatoana na ubora wetu kila timu inataka kuifunga Simba."
Mzambia huyo alisema anajua ligi bado ndefu na kwamba wakitulia na kurejesha majeshi yao Bara ni lazima watu wataelewa anachomaanisha na sio ajabu taji likatua tena Msimbazi kwa mara ya pili mfululizo.


Comments