Usajili wa Haruna Moshi na kukuru kakara za soka ka bongo



Kwangu mimi ni usajili mbovu kwa maendeleo ya soka. Unakumbuka kilichopoteza soka la Italia? Baadhi ya vilabu kung’ang’ania wazee na kuwanyima vijana muda wa kuonesha uwezo. Dunia hii ya sasa Haruna wa nini Yanga?
Usajili huu una mengi ya kujifunza. Yanga inakwenda mbele hatua 5 na kurudi hatua 10. Sio Yanga tu hata upande wa pili wa Simba.
Tumekosea sana kujaza wazee kwenye soka letu kwa kuamini kuwa wataliendeleza soka.
Tusichokijua ni kwamba wachezaji wengi wanaokuja Tanzania sio kwamba ni bora kuliko hawa wakwetu. La Hasha. Mpira una njia zake, unahitaji uwe na kipaji cha uhakika, kujituma kwa bidii zote, na uzoefu/ukomavu wa kutosha.
Wachezaji wengi wa Tanzania wana vipaji na wanajituma ila wengi wao sio wazoefu. Ni kwa sababu hatuwaamini au hatuwapi muda wa kutosha. Tunapenda mchezaji akitoka Mbao akija Yanga msimu wa kwanza atoe asissts 50, afunge magoli 92 ili tuamini anajua. Ni ndoto
Mwisho wa siku Ndemla akipewa msimu mmoja tu asipofanya vizuri msimu unaofuata anafuatwa Niyonzima. Juzi amenunuliwa Mo Rashid lakini hana namba leo katimkia KMC. Labda hapo atapata muda wa kuinua zaidi kiwango chake. Lakini ikumbukwe Mo sio mdogo umri nae haumsubiri. Je lini nae atakuwa na jina lake kwenye mabango ya mashabiki kama tutazidi kuletewa akina Kagere ambao wamecheza zaidi ya mechi 200 tena 50 zikiwa za ligi tofauti tofauti.
Yaani Fei toto tunataka akipewa mechi moja afunge bao 5 na apige chenga kama Messi. Leo akina Chama wanateka vichwa vya habari. Kwanini? Ni kwa sababu yetu rahisi mno. Hakuna mchezaji mzuri atakuja bongo. Aje kufanya nini? Tutaishia kuchukua walioachwa huko ambao hata timu za taifa hawaitwi. Usishangae sana ndo maana Yanga imetoa wachezaji watatu ili kumpata Haruna kama mkombozi wao.
Tumefeli Kwenye nidhamu ya soka ya kuamini katika uzoefu tunachotaka sisi Mimba itungwe leo mtot azaliwe hapo hapo aende shule jioni arudi na degree. Hatupendi kuwapa wachezaji wa ndani muda wa kutosha huku tunawapiga majungu kuwa hawajitumi. Mlitaka wajitume wakiwa benchi? Aliyewaambia mechi 5 zinatosha kuwapima wachezaji ni nani? Na wakati fulani tunataka Ajib ajitume wakati anawadai mamilioni ya hela, yaani apambane ili matumbo ya baadhi ya watu yanawiri wakati mwanae anakosa hela ya pampasi?
Salamba leo anashindana namba na Okwi aliyeanza kucheza ligi kuu Uganda tokea 2004! Hawa wageni wanaokuja sio kwamba wao ni bora sana, hapana, ila waliaminika kwao na walipewa nafasi za kutosha kucheza hivyo wamekwisha kuzoea mpira. Pep alimuondoa Deco na Dinho ili Iniesta na Messi wapate nafasi. Sisi wale wazee wanawaondoa vijana halafu mashabiki watakwambia umri hauchezi mpira.
Usajili wa Haruna unaumiza sana soka letu kama wengi hawajagundua. Haruna ni mtu mzima sana. Wachezaji wengi wa bongo wamedanganyana sana umri. Wengi wanaanzia miaka 26 kuendelea mbele. Mwenye miaka 31 atakwambia ana miaka 24. Najua wanatafuta maisha sina tatizo sana na hilo.
Lakini umri wao unawapumbaza wengi. Yaani mchezaji ana miaka 27 lakini Yanga wao wanajua ana miaka 21 hivyo wanaamini kuwa muda wake wa kukua bado upo. Wanaamini akikaa benchi basi kiwango chake kitakuwa akifikisha miaka 25 atakuwa amekomaa sana.
Kwa akili ya haraka huyu mchezaji akifikisha miaka 25 kiuhalisia atakuwa na miaka 33. Sasa huyu mwenye miaka 33 ndo mnataka aitwe mpaka timu ya taifa? Na katika kipind hiki cha miaka 33 au 35 atakuwa ndo yupo kwenye kiwango kikubwa kwa sababu atakuwa ana uzoefu wa kutosha lakini sasa atakuwa madhara mara mbili, umri wake unamsulubu na bado atakuwa anawasulubu akina Juma Mahadhi wengine wanaokuwa.
Hawa akina Mhilu hawatapewa nafasi kwa sababu kaka yao yupo kwenye kiwango kikubwa. Hivyo Simba na Yanga itakuwa na wachezaji wazee wenye uwezo mkubwa. Lakini uwezo wao sio wa kimataifa ni uwezo wa hapa hapa ndani. Tutakuwa tunawakosa akina Samatta wa baadae.
Simba na Yanga hakuna wachezaji wadogo. Wale wote ni watu wazima tusikimbilie wazee wa nje wakati wazee tunao hapahapa wapewe muda kabla muda haujawapa talaka. Sitaki kutaja mchezaji lakini Boban hajaenda Yanga kawafundisha watoto pale, wale wote ni watu wazima wenye vyeti vya watoto. Tusidanganyane sana. Tunavyozidi kuwaacha benchi kwa kigezo kwamba wajifunze kwa akina Boban ni uongo mkubwa.

Comments