NAANZA MWAKA 2019 NA KABWILI






Na Saleh Ally
MWAKA 2019 utaonekana mpya kwa maana ya namba, lakini mambo mengi sana yatatakiwa muendelezo kama ilivyokuwa kutoka jana kuja leo.

Katika michezo kuna mengi tumepitia na tungepaswa kujifunza wakati tukiandika malengo mengine kwa ajili ya mwaka 2019.

Namba za mwaka zinasaidia mengi, ikiwemo kupata muda wa kujitathmini na kupanga upya yale uliyoteleza kwa ajili ya kuendelea kuishi kwa malengo.

Mengi yaliyo katika michezo yanapaswa kufanyiwa kazi. Migogoro ndio imekuwa ikinikera sana kwa kuwa kwa miaka 20 sasa nikiandika michezo nimekuwa nikiishuhudia na kuipiga vita kutokana na kazi yake.



Ninaamini Mwenyezi Mungu atatuongezea uzima na afya njema na tutaendelea kuelezana ukweli kwa lengo la kuiletea mabadiliko na maendeleo michezo ya hapa nyumbani.

Nimeamua nianze mwaka ikiwa makala yangu ya kwanza naandika kuhusiana na michezo na mtu ninayemlenga ni kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili.

Kabwili ni kipa kinda ikiwezekana kuliko wote wa Ligi Kuu Bara, hii ni kwa maana ya umri na ikiwezekana hata ugeni katika ligi hiyo.

Pamoja na hivyo amekuwa akipata nafasi ya kudaka na katika mechi zaidi ya tano alizodaka akiichezea Yanga, amefanya vizuri na sote tumeona.

Inawezekana kabisa, amekuwa na makosa kadhaa ambayo ungeweza kusema yanatokana na kuwa na uzoefu mdogo wa ligi. Lakini hakuna kati yetu anayeweza kukataa Kabwili ni kipa mwenye kipaji na anaonekana ana mafunzo ya nafasi hiyo.

Kabwili anaweza akawa anafanya vizuri kwa kuwa tu anaonekana ni mtu anayevutiwa sana na kazi yake. Anapenda kuwa mlinda mlango mwenye mafanikio na anafurahia kuwa katika nafasi hiyo.

Nikurudishe mwaka 2018, wakati Kabwili akisajiliwa Yanga niliingia hofu ya yeye kupotea. Nikaeleza ambavyo hofu ilikuwa lakini nikakumbusha ule mfano wa kipa Iker Casillas wa Hispania ambaye alikuwa kipa namba nne wa Real Madrid kabla ya kuibuka na kuwa kipa namba moja tegemeo, shujaa na baadaye gwiji.

Casillas hakutegemea, alijua angeanza kudaka katika kikosi cha kwanza ikiwezekana baada ya misimu minne. Lakini kutokana na suala la makipa wawili kuumia na baadaye mmoja kutaka kuondoka, aliibuka kuwa msaada na baadaye tegemeo.

Hii imejitokeza mwishoni mwa mwaka 2018, sasa ni 2019 naona bado Kabwili ana nafasi. Umeona kipa namba moja aliyekuwa chaguo la Kocha Mwinyi Zahera, Klaus Kindoki alishindwa kudhihirisha hilo. Akaingia Beno Kakolanya ambaye pamoja na kuwa na kiwango kizuri umetokea mgogoro wa suala la malipo, akakaa kando na Zahera akaweka msimamo wake kuhusiana naye.

Baada ya hapo, nafasi imekuwa ni ya Kabwili ambaye pamoja na umri mdogo, uzoefu mchanga lakini amekuwa akiitendea haki.

Yanga ina presha kubwa kutokana na suala la kifedha licha ya kwamba wanachama na mashabiki wamekuwa wakijitahidi katika uchangiaji na kuupunguza. Lakini Kabwili anaonekana anazidi kuihimili presha hiyo na kuonyesha kiwango chake.

Wanayanga lazima wakubali kwamba wamepata bahati ya kuwa na kipa kinda mwenye kipaji cha juu. Tena ambacho kinavutia zaidi, kipa huyo ni Mtanzania na kama ataungwa mkono, tunaweza kutengeneza kipa mwingine gwiji kama ilivyokuwa kwa akina Juma Pondamali, Mohammed Mwameja, Iddi Pazi hadi Juma Kaseja.

Nakukumbusha tena, Kabwili ni kipa Mtanzania ambaye kesho atakuwa chagizo la vijana wengine kujituma, kujiamini kwenda katika mafanikio.

Hivyo tumuunge mkono ili kuhakikisha kipaji chake kinakuja kuwa faida kwa taifa letu. Kitakuwa faida kama ataendelea kufanya vizuri kwa kuwa amepata bahati ya kuwa na msingi mzuri kuanzia mapema.

Msingi aliopata ni pamoja na ule wa kimataifa. Na ukiangalia umri wake ambao ni mwanzoni mwa miaka 20, maana yake ana miaka mingine takribani 20 ya kuendelea kucheza na kama akiendelea kujengwa vizuri leo, basi atakuwa hazina na faida katika taifa letu.

Binafsi nilikutana naye alipofika ofisini kwetu kwa mahojiano na Global TV Online na kumueleza hivi kwamba, tunamuunga mkono, tunatamani afanikiwe na tungependa awe chagizo la vijana wengine kutaka kufanikiwa.

Ninaamini kuna siku Kabwili atakosea, kama itatokea tunaweza kumueleza lakini tusifanye hukumu ya kummaliza. Sisi Watanzania kama tutaweka pembeni ushabiki na kuangalia uendelezaji wa michezo yetu, basi niwakumbushe, tunahitaji kuwapa sapoti wanamichezo wetu kwa kusema ukweli na kuwaelekeza njia iliyo sahihi.

Kabwili ana nafasi ya kutengeneza maisha yake, kusaidia Yanga lakini kulisaidia taifa letu na wapenda michezo wengine wakiwemo wale wanaochipukia.

Heri ya mwaka mpya wanamichezo wote.

Comments