MWENDO WA LIGI KUU KWA SASA UNATIA MASHAKA MAKUBWA HASA KWA UPANDE WA WAAMUZI, HATUA STAHIKI ZICHUKULIWE


KAMA ambayvo unaskia kwa sasa ni mwendo wa kila mmoja kushinda mechi zake ambazo anazo mkononi mwake hivyo hiyo ni falsafa ambayo inapewa kipaumbele na kila timu.

Wale ambao bado wanadhani wapo mzunguko wa kwanza kwa sasa ni wakati muafaka wa kuzinduka na kuanza kufanya kweli kwa michezo iliyobaki.

Ukweli utabaki palepale kwamba mwenye kisu kikali ndiye atakula nyama kwa jinsi hali ilivyo ndani ya ligi hivyo kwa yule ambaye anatambua ana mechi mbele hakuna kitu kama hicho.

Kitaalamu tunasema tupo kwenye wakati wa mavuno ambapo kila mtu atavuna kile alichokipanda hasa inapofika mwisho wa mzunguko wa pili.

Maandalizi kwa timu zote yanapaswa kuwa yanayokwenda na uhitaji wa benchi la ufundi bila kuhusisha viongozi ambao jukumu lao ni kuona wanatimiza matakwa ya wachezaji wao pamoja na benchi la ufundi.

Mechi nyingi kwa sasa zimekuwa na matumizi makubwa ya nguvu jambo ambalo sio sawa hasa ukizingatia kwamba mchezo wa miguu ni mchezo wa amani.

Wengi wanashindwa kutambua kwamba kwa sasa kinachosumbua ni hii ngwe ya lala salama kila mmoja hesabu zake ni kuona anapata pointi tatu kibindoni zitakazomfanya afikishe lengo lake.

Hapo ndipo mbinu mbovu zinaanza kutumika ili kupata matokeo, hili jambo sio sawa haina maana kwa afya ya soka letu ambalo kila iitwapo leo linapiga hatua taratibu kuelekea kule kwenya mafanikio.

Ubabe ambao unatokea Uwanjani vitendo vya kuonyesha mabavu uwanjani hata vile vitendo ambavyo hutumika katika uwanja visivyo vya kinidhamu ni vibaya na vinapaswa vikemewe kwa vitendo.

Tunashuhudia matukio ambayo tulishaanza kuyasahau yakianza kutokea tena Uwanjani hili halikubaliki ni wakati wa benchi la ufundi kushtuka na kukaa na wachezaji kuwafundisha nidhamu.

Umakini kwa wachezaji na waamuzi ni jambo la msingi, wote lazima waamue kutenda haki katika michezo yote wanayocheza kwa upande wa wachezaji na waamuzi kusimamia haki kwa michezo wanayosimamia.

Wachezaji wanapaswa wawe makini na kila wanachokifanya Uwanjani ili kisiigharimu timu hasa kwa kutenda vitendo visivyo vya kinidhamu ambapo matokeo yake ni kuzawadiwa kadi ya njano ama nyekundu hii si sawa.

Kuna makosa ambayo yanaweza kuzuilika kabla ya kuyatenda kwa mchezaji mwenyewe hivyo ni muhimu kuzingatia sheria na kununi za mpira.

Upande wa waamuzi hili la lawama sasa linapasua vichwa vya wengi, kwani kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa sasa hata timu inayoshinda nayo pia ina mgeukia mwamuzi hili ni jambo la hatari.

Kama kila mmoja anampigia hesabu mwamuzi ina maana kuna hatari ambayo ipo kwa waamuzi wetu hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa litazame hili kwa jicho la pekee.

Ushindani uliopo kwa sasa umeanza kupoa kwa kiasi fulani ni jambo linaloongeza hatari, mashabiki wanahitaji kuona ushindani wa kweli na mkubwa kwenye ligi yetu.

Ujanjaujanja wa wachezaji kutafuta matokeo uwanjani hili halijakaa sawa kinachohitajika ni ushindani wa kweli na kila mmoja apambane kutafuta matokeo.

Waamuzi bado hampaswi kulikwepa zigo la lawama ambalo mnapewa kwa sasa bali ni wakati muafaka wa kuwazindua na kuwafanya mtambue kwamba muda uliopo wa ujanja una kikomo chake.

Zindukeni kwa yale ambayo mnayafanya yasiyo sawa kisheria kwani wahenga walisema lisemwalo lipo na kama halipo basi laja.

Mdudu rushwa kwenye michezo yetu asipewe nafasi hasa kutokana na ukata ambao unazikumba timu nyingi kutokana na kukosa mdhamini mkuu wa ligi.

Tusitumie ukata kama fimbo ya kuwachapia wale ambao hawana uwezo katika kujiendesha na kuamua kutengeneza matokeo Uwanjani hili halitujengi.

Kwa sasa kila timu ishinde kwa mbinu uwanjani na uwezo na ule ujanja ambao unatumika kwa baadhi ya timu uachwe mara moja hesabu zetu ni kuona tunapata bingwa ambaye anakuwa halali na sio wa mezani.

Wakati wetu wa kuwa na ligi bora ni sasa hili duru la lala salama lisitufanye tusahau tulikotoka, mchezo wa mpira usiwe sehemu ya kisasi bali iwe ni sehemu ya furaha kwa pande zote mbili.

Kutoka Championi

Comments