NANI ANAMPA KIBURI MWAMUZI HUYU BONGO? ANA TABIA ZA AJABU KINOMA AKIWA KAZINI

JONESIA Rukyaa mwamuzi mwenye beji ya Fifa ambaye kwa sasa naona kadri siku zinavyzidi kwenda anapunguza ule umakini wake kwenye utendaji wa kazi akiwa Uwanjani.
Hakuna ubishi kwamba miongoni mwa marefa ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mechi ambazo wanazisimamia alikuwa ni miongoni mwao ingawa alikuwa na mapungufu yake.
Wengi huwa wanamkubuka kutokana na kuchezesha mechi kubwa na ngumu kwa Ligi Kuu Bara ambazo ni Simba na Yanga hali ambayo ghafla ilimpa umaarufu na kuwa gumzo kila kona.
Kwa namna Ligi Kuu Bara inavyokwenda matarajio ya wengi ni kuona waamuzi wanakuwa mstari wa mbele kutetea haki hasa kwa kufuata sheria 17 za mpira ila ajabu wao wanageuka waasi namba moja.
Ni waasi namba moja kutokana na ukweli ulivyo tena kwa mechi zinazoonyeshwa live kuna madudu sasa zile ambazo hazionyeshwa live ndio zina madudu kupitiliza yale yanayoonekana.
Hebu nikukumbushe kidogo namna halisi ya kile ambacho ninakizungumzia leo, kwa wenye kumbukumbu nadhani bado mnakumbuka tukio la mwamuzi Jonesia kuonyesha ubabe mbele ya mlinda mlango wa Mtibwa Sugar.
Benedick Tinoco, ni miongoni mwa magolikipa warefu Tanzania na ni mtu mwenye jeuri hasa inapofikia maamuzi yasiyo ya lazima ila nilishangazwa kibao kilivyogeuka naye akawa mpole mbele ya Jonesia.
Tukio lilionekana kupitia Azam TV ambapo mwamuzi alimfuata mlinda mlango na kumsukuma kwa kifua chake, hii inamaanisha nini? Kwa walimu tunatambua kwamba maana halisi ya kitendo kile ni ubabe na jeuri.
Ulimwenguni kote mwamuzi ni mtu ambaye jukumu lake ni kutimiza sheria 17 masuala ya ubabe na jeuri sasa vinatoka wapi kwetu sisi wabongo ambao bado tunajikongoja?.
Kumbuka kwamba huo ulikuwa ni mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika 'FA' sasa mambo hayo waamuzi wameamua wahamishie pia kwenye Ligi Kuu Bara kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litaendelea kukaa kimya hii ni hatari.
Ghafla tu kuna mdudu mwingine ambaye anaendelea kumfuata Jonesia mpaka kwenye ligi aendelee kusambaa na tabia yake ambayo sio sawa hasa kwa mwalimu ambaye anatambua sheria na namna mpira unavyotakiwa kwenda.
Nakumbuka mchezo wa Lipuli na Kagera Sugar matokeo yalikuwa mabaya kwa upande wa Lipuli ila nyuma ya pazia waamuzi walikuwa wanashangilia kwa kuwa walikuwa hawajali.
Mabao yote mawili ambayo yameingia kwenye nyavu ni ya kuotea bila chenga ila sasa hakuna anayeshtuka sio mwamuzi wa kati wala mshika kibendera hii ni hatari kwa ligi yetu.
Ajabu kubwa hata wachezaji wa timu pinzani wao wenyewe hawaelewi ni kwa nini wanashinda zaidi ya kuishia kusema kwamba wapo kwenye hali mbaya.
Hii inaleta taswira mbaya kwa timu pamoja na wachezaji kuona kwamba ukiwa ugenini ni lazima unyimwe haki yako hata kama utacheza kwa umakini na kutumia nafasi sawasawa.
Jonesia pia amehusika katika hili akiwa kwenye benchi kwa nafasi ya kamisaa wa marefarii hakuwa tayari kusikiliza malalamiko ya mwalimu zaidi ya kuishia kutumia nguvu na kutoa maneno ambayo sio sawa.
Hapo ndipo utajua kwamba kwa sasa mazingira ya mshindi yanapangwa, tena hali ni mbaya zaidi kwa mechi ambazo hazionyeshwi unachinjwa mzimamzima bila kukutazama.
Kiukweli TFF kwa maendeleo ya soka letu ni muhimu kuona namna gani haki itapatikana kwa timu shiriki hasa zile ambazo hali zao kiuchumi ni za kuunganishaunganisha, inaleta hasira kuona haki inapotea.
Tazama pia kwa upande wa timu za kanda ya ziwa bado waamuzi wanatoka maeneo hayo, maumivu ni makubwa, sitaki kuhusisha matokeo ya uwanjani na masuala ya rushwa ila haki inaminywa waziwazi kwa timu za chini.
Ninachojiuliza huu ubabe wa Jonesia anaupata wapi na kwa nini anakuwa na tabia za namna hii ilihali ni msomi anayetegemewa hasa kwenye mpira?
Jeuri anayoonyesha kwa walimu nayo anaipata wapi ilihali ameaminiwa na kupewa majukumu ya kusimamia sheria 17 za michezo?.
Hakuna timu kwa sasa ambayo inakubali kupoteza kiwepesi ni kweli walimu wote hawana lengo la kupoteza je wanapoteza kwa mazingira ya aina gani na kama wanaonewa basi kuna haja ya kutazama kwa ukaribu malalamiko yao.
Waamuzi ni vema tuakaacha tabia za ubabe na kuchezesha mpira kwa kufuata kanuni hali itakayofanya tupate washindani wa kweli kwenye soka letu.
Timu nyingi zinahaha kutafuta matokeo ila zinapokuwa ugenini zinakutana na kikwazo kinachowafanya wapoteze kwa lazima.
Kama hili halitatazamwa tutashuhudia mengi mzunguko wa pili ambao umeanza kwa sasa ikiwa ni lala salama kwenye ligi yetu Tanzania Bara ambayo haina mdhamini mkuu.
Waamuzi watende haki bila kubagua aina ya mchezo na viongozi wa timu pia waache mtindo wa kuwakandamiza wageni, hili ni soka tunahitaji kuona wachezaji wakipambana uwanjani na si nje ya Uwanja.
Kutoka Championi

Comments
Post a Comment