AZAM FC YAICHAPA MADINI 2-0 NA KUINGIA HATUA YA 32 BORA KOMBE LA TFF



TIMU ya Azam FC imetinga hatua ya 32 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuichapa Madini FC mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumapili usiku.
Licha ya ushindi huo wa Azam FC, kwa hakika ilikutana na ushindani mkubwa kutoka kwa Madini ambayo ilionekana kujilinda vema na kuwazuia matajiri hao kwa muda wa dakika 66 za mchezo huo.
Baada ya kosakosa nyingi za kipindi cha kwanza, hatimaye shambulizi zuri lililofanywa dakika ya 67 liliipa bao la uongozi Azam FC likifungwa na winga Enock Atta, kwa kichwa akimalizia krosi ya mshambuliaji Obrey Chirwa.
Chirwa alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Azam FC kwenye mechi rasmi ya mashindano tokea asajiliwe katika dirisha dogo la usajili lililofungwa hivi karibuni kwa usajili huru akitokea Nogoom ya Misri.
Zayd aliyeingia dakika ya 57 kuchukua nafasi ya winga Idd Kipagwile, alifanikiwa kufunga bao la kiufundi dakika ya 84 kwa shuti zuri nje ya kidogo ya eneo la 18 akimalizia pasi ya beki wa kushoto Bruce Kangwa.
Katika mchezo huo, Azam FC ilipata pigo dakika ya 36 baada ya kuumia kwa kiungo wake Tafadzwa Kutinyu, ambaye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Stephan Kingue, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza tokea arejeshwe kwenye usajili wa dirisha dogo.
Baada ya ushindi huo kikosi cha Azam FC kitasubiria kupangiwa mpinzani wake kwenye raundi ijayo, ikikutana na moja ya timu zilizopenya kwenye raundi ya tatu.   
Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuendelea na mazoezi kesho asubuhi, tayari kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Manungu Desemba 29 mwaka huu saa 10.00 jioni.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Aggrey Moris, Mudathir Yahya, Idd Kipagwile/Yahya Zayd dk57, Tafadzwa Kutinyu/Stephan Kingue dk36, Donald Ngoma/Ramadhani Singano dk70, Obrey Chirwa, Enock Atta-Agyei.

Comments

Popular Posts