KOMBE LA MAPINDUZI KUANZA JANUARI 1, YANGA NA AZAM KUNDI MOJA



MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2019 imepangwa kuanza Januari 1 hadi 13, mwakani ikifanyika katika miji ya Pemba na Unguja.
Jumla ya timu tisa zitashiriki michuano hiyo, sita kutoka Zanzibar ambazo ni KVZ, KMKM, Jamhuri, Chipukizi, Mlandege na Malindi wakati tatu ni za Tanzania Bara ambazo ni Azam, Simba na Yanga.
Timu hizo zimepangwa katika makundi mawili ambapo Kundi A linajumisha timu za Chipukizi, Mlandege, KMKM na Simba wakati Kundi B litakuwa na timu za KVZ, Malindi, Jamhuri, Azam na Yanga.
Kama ilivyo kawaida, mechi zote za mashindano hayo zitaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam kupitia chaneli zake mbalimbali.
Na Kamati ya maandalizi ya mashindano hayo imesema kuwa zawadi kwa mshindi wa kwanza itaongezwa kutoka shilingi milioni 10 hadi kufikia shilingi milioni 15 ikiwa ni pamoja na medali za dhahabu pamoja na kombe.
Mshindi wa pili naye naye atapata shilingi milioni 10 badala ya milion 5 iliyokuwa ikitolewa awali, na medali za fedha.
Kama Azam FC watachukua kombe hili mwaka huu wa 2019, Kombe litakuwa ni mali yao kwa mujibu wa kanuni kwani watakuwa wamelichukua kwa miaka mitatu mfululizo.
Mashidano hayo msimu huu yatafanywa katika Uwanja wa Amaan uliopo Unguja kwa mechi zote hadi Nusu Fainali na mchezo wa Fainali utafanyika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.
Mechi za Amaan zitakuwa zinachezwa kuanzia Saa 10:15 jioni na Saa 2:15 usiku huku mechi ya fainali ikitarajiwa kuchezwa kuanzia Saa 9:30 Alasiri.


Comments

Popular Posts