NAMNA CHAMA ALIVYOWASHTUA CAF



KIUNGO wa Simba, Clatous Chama, ameweka rekodi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushika nafasi ya pili kwenye chati ya ufungaji akiwa ni mchezaji pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf), limeweka listi ya wachezaji wanaoongoza kwenye chati ya ufungaji huku mchezaji huyo raia wa Zambia akishika nafasi ya pili baada ya kufunga mabao manne akizidiwa na Moataz Al-Mehdi wa Al Nasr ambaye ana mabao sita.

Chama ameweka rekodi hiyo, akiwa ndiye kiungo pekee kwenye listi hiyo kuanzia mchezaji wa kwanza hadi yule anayeshika nafasi ya nane kwenye chati hiyo ya ufungaji katika michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

Chama ambaye amekuwa gumzo, alianza kwa kuwafunga Mbabane Swallows ya Eswatini, ambapo nyumbani alifunga bao moja na ugenini alifunga mawili, lakini pia Jumapili iliyopita alifunga bao lingine kwenye ushindi wa Simba wa mabao 3-1 dhidi ya Nkana FC ya Zambia.

Listi hiyo ya ufungaji inaonyesha kuwa Simba ndiyo timu pekee ambayo ina wachezaji watatu kwenye kumi bora. Wachezaji wengine wa Simba ni Meddie Kagere ambaye anashika nafasi ya saba akiwa na mabao matatu na John Bocco anayeshika nafasi ya kumi kwenye ufungaji akiwa nayo mawili.

Hii inaonyesha kuwa Simba ndiyo wapo vizuri zaidi kwa sasa katika ufungaji. Katika listi hiyo hadi mchezaji wa 11, hakuna timu ambayo imetoa wachezaji wenye mabao kuanzia mawili zaidi ya Simba.

Chama ameonekana pia kuweka rekodi nyingi akiwa ndiye mchezaji pekee aliyehusika kwenye mabao yote matatu ya Simba katika mchezo dhidi ya Nkana.

Mzambia huyo alitoa pasi ya bao la kwanza ambalo lilifungwa na Jonas Mkude, lakini pia alihusika kwenye bao la pili ambapo alitoa pasi kwa Nicholaus Gyan ambaye alimpasia Kagere aliyefunga kwa ustadi mkubwa akitumia kichwa.

Lakini pia Chama alihusika kwenye bao la tatu la timu yake ambapo alipata pasi murua kutoka kwa Hassan Dilunga na kufunga kwa kisigino likiwa ni bao ambalo lina nafasi kubwa ya kuwania Tuzo ya Bao Bora la Mwaka la Afrika.

Lakini mbali na hilo pia kiungo huyo ana pasi mbili za mabao, asisiti ambapo alitoa moja kwenye mchezo dhidi ya Mbabane kwa bao lililofungwa na Kagere.

Sasa Simba watapambana na TP Mazembe, Al Ahly, Wydad Casablanca, Espérance, Mamelodi Sundowns, AS Vita Club, Horoya, Club Africain, ASEC Mimosas, Orlando Pirates, CS Constantine, JS Saoura, Ismaily, Lobi Stars na FC Platinum ambazo zimefanikiwa kufuzu kwa hatua hiyo ya makundi

Comments

Popular Posts