BIASHARA UNITED YAENDELEA KUNG'ARA CHINI YA AMRI SAIDI, YAIPIGA COASTAL 3-2



TIMU ya Biashara United ya Mara imeendelea kufanya vyema chini ya kocha mpya, Amri Said ‘Stam’ baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Karume, Musoma.
Mabao ya BUM leo yamefungwa na George Makanga dakika ya 21, Innocent Edwin dakika ya 61 na Juma Mpakala dakika ya 85, wakati ya Coastal Union ya kocha Juma Mgunda yamefungwa na Hamisi Kanduru dakika ya 12 na Hajji Ugando dakika ya 65.
Kwa ushindi huo, Biashara United inafikisha pointi 17 baada ya kucheza mechi 20, ikijiinua hadi nafasi ya 18 kutoka mkiani kabisa, nafasi ya 20, wakati Coastal Union inabaki na pointi zake 25 katika nafasi ya nane baada ya kucheza mechi 19.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, wenyeji Mbao FC wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya jirani zao, Stand United ya Shinyanga Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. 
Mabao ya Mbao FC iliyo chini ya kocha Ally Bushiri yamefungwa na Rajesh Kotecha dakika ya 13 na Pastory Athanas dakika ya 45 na ushei, wakati la Stand United limefungwa na Mwinyi Elias dakika ya 63.
Mbao FC inafikisha pointi 30 baada ya kucheza mechi 21, ingawa inabaki nafasi ya sita wakati Stand United inayobaki na pointi zake 22 baada ya kucheza mechi 21 inabaki nafasi ya 16.
Mchezo kati ya wenyeji, Mbeya City na Mtibwa Sugar uliokuwa ufanyike leo pia umeahirishwa hadi kesho kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha leo kuharibu mandhari ya Uwanja.


Comments

Popular Posts