Huyu ndiye Arthur Melo anayejua kuuficha mpira.
Jina la Arthur Melo halizungumzwi sana kwenye vyombo vya habari kwasababu kiungo huyo bado hajaonekana ni mtu muhimu kwa Klabu ya Barcelona. Baada ya Xavi Hernandez kuondoka, sikutegemea kama Barcelona watazalisha kiungo mwingine mwenye ubora kama wa Xavi. Ni ngumu sana kumpata mchezaji kama Xavi kwa kizazi cha sasa. Simaanishi Arthur Melo amesajiliwa awe mbadala wa Xavi, hapana ila staili ya uchezaji haitofautiani sana na Xavi Hernandez.
Kuna watu wengine wanaamii kwamba Arthur Melo, sio muhimu sana kwasababu yupo pia kiungo Denis Suarez. Kinachombeba Denis Suarez ni namna anavyochangia kutoa passi za magoli pamoja na kufunga. Ukiangalia hizo sifa, huwezi kuona kama kuna kitu kingine ambacho ni muhimu zaidi. Ubora wa Arthur Melo ni kuifanya timu ikae na mpira( kumiliki mpira) kupunguza kasi ya timu pinzani isikushambulie sana. Msingi mkubwa wa timu, ni katika safu ya kiungo. Bila kuwa na Arthur Melo, mwenye uwezo wa kuituliza timu, usitegemee utakuwa na hali ya kujiamini kwenye eneo la tatu na la mwisho wa uwanja. Mipango inaanzia kwenye safu ya kiungo halafu ndipo utaona assist na magoli yanafata.
Mara nyingi timu inayocheza kwa nguvu kubwa kipindi cha kwanza halafu nguvu ikapungua kipindi cha pili basi ujue haina mtu kama Arthur Melo. Arthur, akisema aufiche mpira, anauficha kweli na timu inakuwa mchezoni. Kama Arthur yupo uwanjani hutegemei kuona Barcelona ikikaribisha mashambulizi mengi. Barcelona hata ikiwa imetangulia kwa magoli mawili au matatu, bado itakuwa bora kwenye kuutawala mchezo. Anajua namna ya kuuliza maswali kwa timu pinzani ili apate nafasi ya kupiga passi kwenda kwa wachezaji wenzake.
Timu ambazo hazina kiungo aina ya Arthur, zinakuwa na wakati mgumu kwenye kuua mechi au kushinda mechi bila shida yoyote. Unakuta mfano timu kama Man United inacheza kwa kiwango kizuri kipindi cha kwanza lakini nguvu iliyotumika kipindi cha kwanza huioni kipindi cha pili kwasababu ina viungo ambao wana akili ya kuzuia sana kuliko kuituliza timu isikaribishe mashabulizi mengi.
Barcelona haikuona tatizo kuwapa Gremio milioni 31, ili ipate huduma ya Arthur Melo. Walihitaji mchezaji aina ya Xavi. Ni kiungo ambaye ni mara chache sana kumuona katika timu nyingi kwa sasa. Ana safari ndefu ya kuendelea kutufanya tuamini uwezo wake maana bado ana umri mdogo sana.
Comments
Post a Comment