POPADIC KOCHA MPYA SINGIDA UNITED, MSAIDIZI WAKE MSERBIA PIA, DUSAN


WALIOWAHI kuwa makocha wa Simba SC kwa wakati tofauti, Dragan Popadic na Dusan Momcilovic wamejiunga na klabu ya Singida United.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Singida United imewatambulisha makocha hao wawili raia wa Serbia ikisema Popadic atakuwa kocha mkuu na Msaidizi wake, Momcilovic.   
Popadic alipata umaarufu mkubwa wakati akiifundisha klabu ya SImba SC kati ya mwaka 1994 na 1996 kabla ya kuondoka, wakati Momcilovic alikuwa Msaidizi wa kocha Muingereza, Dulan Kerr katika klabu hiyo mwaka kati ya mwaka 2015 na 2016.
Wakati Popadic ni mwalimu kamili na aliyebobea katika soka ya Afrika, Momcilovic ni kocha wa mazoezi ya viungo wa kiwango cha juu pia.
Singida United inaajiri Waserbia hao kiasi cha miezi saba tangu iachane na kocha wake Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyehamia Azam FC.
Ikumbukwe baada ya kuondoka Pluijm ambaye walimchukua kutoka klabu ya Yanga pia ya Dar es Salaam, Singida United walimchukua Kocha Mzanzibar, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye hata hivyo hakudumu.
Kwa muda sasa timu ipo chini ya Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na klabu ya Yanga, Nsajigwa Shadrack.
Kwa sasa Singida United inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi zake 24 baada ya kucheza mechi 20.   
Na imefanikiwa kutinga hatua ya 32 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambako itamenyana na JKT Tanzania ambayo ikifanikiwa kuitoa itakutana na mshindi kati ya Kitayose na Coastal Union katika 16 Bora.

Comments

Popular Posts