STAND YAIWEKA KANDO YANGA, HESABU ZAO HIZI HAPA
KOCHA wa Stand United, Amars Niyongabo amesema kuwa baada ya kuifunga Yanga mchezo wao wa Ligi Kuu kwa sasa akili zao wanazihamishia kwenye mchezo wao ujao wa kombe la Shirikisho.
Yanga wamevunja mwiko wao wakiwa ugenini mbele ya Stand United baada ya kufungwa bao la usiku na Jocob Masawe dakika ya 88 na kufanya washindwe kuendeleza kulinda rekodi ya kufikisha mchezo wa 20 bila kufungwa.
Niyongabo amesema walitambua ubora wa Yanga umejificha kwenye mipira ya haraka pamoja na ubora wa kutumia faulo wanazozipata eneo la hatari hivyo baada ya ushindi huo akili zao wanazipeleka kwenye mchezo wa FA.
"Tulijua tunacheza na timu ya aina gani ambayo ukiangalia ubora wao upo kwenye kutumia mipira iliyokufa pamoja na mashambulizi ya kushtukiza hivyo wachezaji wangu wote niliwapa kazi maalumu ya kutembea na wale wachezaji wagumu na kuwafuata kwa nidhamu ndani ya Uwanja.
"Tumefanikiwa katika hilo, tunasahau kuhusu Yanga na ushindi wetu tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wetu wa FA ambao tutacheza na timu ya Rhino mkoani Tabora," alisema Niyongabo.
Kombe la FA kwa sasa lipo mikononi mwa Mtibwa Sugar ambao walibeba msimu uliopita baada ya kuibuka washindi mbele ya Singida United.
Comments
Post a Comment