UHAKIKA ALIOUTAJA KOCHA SIMBA KABLA YA KUMALIZANA NA AS VITA JUMAMOSI
KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema kuwa kikosi chake kipo imara kuwavaa AS Vita na wana uhakika wa kuibuka na ushindi kutokana na maandalizi waliyofanya.
Simba watamenyana na AS Vita ya Congo, Jumamosi ikiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa wakiwa na kumbukumbu ya kuanza kwa ushindi mbele ya JS Saoura ya Algeria huku wapinzani wao wakiwa na maumivu ya kupoteza mchezo wao wa kwanza hatua ya makundi.
Aussems amesema anawatambua wapinzani wake kwa kuwa alipata muda wa kuifuatilia timu hiyo na amegundua ni timu bora haipaswi kubezwa wao wanaifuata kishujaa.
"Tumeanza vizuri ina maana morali ya wachezaji ni kubwa, kazi yetu iliyo mbele yetu ni kuona tunafikia malengo kwa kupata matokeo pia kwenye mchezo wetu wa ugenini bila kuwa na hofu yoyote, hilo linawezekana.
"Kipaumbele kwa wachezaji wangu ni kuona tunapata matokeo kwenye mchezo wetu kwa hali na mali, hali ambayo imenifanya niwape wachezaji mbinu kali zitakazotufanya tupate matokeo, nimewaambia wachezaji nataka mabao ya mapema ili kufanikiwa kuumudu mchezo," alisema Aussems.
Simba wameondoka leo kuwafuata wapinzani wao AS Vita ambao wapo nao kundi D ambalo kwa sasa Simba anaongoza kwa kuwa na idadi ya mabao matatu akifuatiwa na All Ahly ambao wana mabao mawili, As Vita na JS Saoura hazina pointi.
Comments
Post a Comment