Yanga, Mtibwa kuweka historia au kumpisha Azam FC?
HATUA ya 32 bora katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam imepangwa kuchezwa kati ya Januari 25 hadi 28 mwaka huu kwa timu hizo kuchuana kutafuta nafasi ya kutinga mzunguko wa 16 bora.
Kulingana na droo hiyo iliyozechezwa Alhamisi iliyopita mubashara kwenye kituo cha Televisheni cha Azam iliyoshirikisha timu 32 kutoka Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, mabingwa watetezi wa kombe hilo Mtibwa Sugar wamepangwa kucheza na Majimaji FC uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.
Yanga watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwakaribisha Biashara United ya mkoani Mara wakati Azam FC wao wakiwaalika Pamba FC ya Mwanza ndani ya dimba la Chamanzi Complex .
Mashujaa FC iliyowatoa, Simba itacheza nyumbani dhidi ya Mbeya Kwanza dimba la Like Tanganyika, KMC ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Pan Africans.
Rhino Ranges itakuwa wenyeji mbele ya Stand United , wakati Mbeya Kwanza wao watakuwa wageni kwa Kagera Sugar dimba la Kaitaba mjini Bukoba.
Polisi Tanzania ya Ligi daraja la Kwanza wataikaribisha Lipuli FC ya TPL, Coastal Union wao watakuwa wageni kwa Kitayosa FC huku Singida United kwa mara nyingine tena atakuwatana na JKT Tanzania.
Kwa upande wa African Lyon wao watakutana na Friend Ranges dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam, Alliance wao watakuwa wenyeji wa La Familia wakati Transit Camp watakuwa wenyeji kwa Dodoma FC.
Raundi hiyo 32 bora itaitimishwa kwa mchezo kati ya The Mighty Elephant vs Namungo FC wakati Reha FC wao watawaarika Boma FC huku Dar City wakiwaalika Cosma.
Mshindi katika michezo hii ataingia hatua ya 16 bora kabla ya kucheza nane bora kisha nne na hatimae fainali ambayo kwa mwaka huu imepangwa kuchezwa ndani ya Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.
Kama ilivyo kawaida kwa miaka mitatu mfululizo bingwa wa mashindano haya anaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani.
Tangu kuanza kwa mashindano haya, ni Yanga, Simba na Mtibwa Sugar ndio waliofanikiwa kulichukua taji lakini kwa mwaka huu kunaonekana kuwa na kitendawili iwapo kama Yanga na Mtibwa wataweka rekodi ya kuchukua mara mbili hasa baada ya Simba kutolewa mapema mashindanoni.
Lakini pia vipi kuhusu Azam FC, Singida United na timu nyingine za Ligi Kuu nafasi yao katika mbio hizo kulingana na historia iliyopo ya kuwa ni timu za TPL pekee ndio wanalotwaa taji.
Msimu uliopita fainali ilichezwa kati ya Mtibwa Sugar na Singida United ambao nao watakuwa na kiu ya kutwaa taji hilo baada ya kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ukiondoa timu za TPL zipo pia za FDL pamoja na SDL ambazo zote zinauwezo wa kubadili matokeo yoyote na kusonga mbele ingawa ukweli ulio wazi za Ligi Kuu wana nafasi kubwa ya kuendeleza ubabe wao wa kuchukua taji hilo japo lolote linaweza kutokea kwenye mchezo wa soka.
Licha ya uwepo wa timu hizo za Ligi Kuu lakini bado ushindani umezidi kuwa mkubwa kutoka klabu zinazoshiriki ligi za chini kwa kiasi kikubwa inaonyesha jinsi gani soka la Tanzania limepiga hatua.
Hata katika nchi zilizoendelea ni suala la kawaida kwa timu za madaraja ya chini kushinda dhidi ya zile zilizopo Ligi Kuu kama ilivyoonekana hivi karibuni Mashujaa FC walipoifunga Simba.
Comments
Post a Comment