AZAM FC WANA SHUGHULI PEVU FEBRUARI HII, MECHI SITA TATU UGENINI
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeonekana kuwa na ratiba nzito mwezi Februari mwaka huu.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa, Azam FC itacheza jumla ya mechi sita, tano zikiwa za Ligi Kuu na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ikitarajia kucheza nyumbani kukipiga na Rhino Rangers kati ya February 22 na 25 mwaka huu.
Azam FC kwenye ratiba hiyo itaanza kukipiga na Alliance nyumbani, Jumatano ijayo saa 1.00 usiku kabla ya kucheza mechi tatu mfululizo ugenini, ikianzia mkoani Iringa kukipiga na Lipuli Februari 11.
Baada ya mchezo huo itasafiri hadi jijini Mbeya kuvaana na Maafande wa Tanzania Prisons, utakaofanyika Uwanja wa Sokoine Februari 14, siku nne baadaye itatakiwa kuvaana na Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Aidha ikimalizana na Coastal, Azam FC itatakiwa kurejea jijini Dar es Salaam kuvaana na Simba, ikiwa mwenyeji wa mchezo huo, lakini ikiwa tayari imefanya uamuzi wa kutumia Uwanja wa Taifa, katika mechi zote dhidi ya Wekundu hao na Yanga.
Ratiba ya Azam FC ya mwezi huo itamalizika kwa Azam FC kurejea Uwanja wa Azam Complex kusaka robo fainali ya Kombe la FA, itakapochuana na maafande wa Rhino Rangers.
Tayari kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mechi hizo, kocha wake, Hans Van Der Pluijm, akiwa amejipanga vema kufanya vizuri katika mechi zote hizo.
Wachezaji waliokuwa wagonjwa, kiungo Tafadzwa Kutinyu na beki David Mwantika, wamerejea mazoezini wiki hii tayari kuimarisha kikosi hicho kuelekea kwenye vita ya mechi hizo.
Comments
Post a Comment