Askari Polisi afia Bar akiwa tungi kichwani, wahudumu waeleza kilichomsibu dakika za mwisho
Askari Polisi mmoja mkoani Ruvuma, amekutwa amekufa kwenye Bar ya Friend’s Pub iliyoko katikati ya mji wa Songea huku ikielezwa kuwa alikuwa amekunywa pombe kupita kiasi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Machi 15, 2019 ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa, alimtaja askari polisi aliyekutwa amekufa kuwa ni Konstebo Donald Motoulaya (29), ambaye ni askari katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa.
Kamanda Marwa amesema kuwa, siku ya tukio hilo, juzi majira ya saa 4:15 asubuhi, Jaibu Nyoni (26) ambaye ni mhudumu wa Bar hiyo, alitoa taarifa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi kuwa askari Donald amelala kwenye kochi na amejaribu kumwamsha lakini imeshindikana.
Kamanda Marwa alifafanua zaidi kuwa, baadaye askari waliongozana na daktari kwenda eneo la tukio ambako walimkuta askari huyo akiwa amelala kwenye kochi ambalo liko ndani ya bar hiyo.
Marwa amesema katika uchunguzi ilibainika kuwa askari huyo alifika kwenye baa hiyo Machi 12, majira ya saa 4:30 usiku akitokea katika Bar nyingine iitwayo Mtini Pub, ambako alikuwa akinywa pombe.
Mtoa taarifa alieleza kwamba wakati askari huyo anaingia Friend’s Pub, aliteleza na kuanguka kwenye ngazi na baadaye alimwinua na kumtoa nje kisha askari huyo alirejea na kukaa kwenye kochi wakati huo mhudumu akiendelea kuhudumia wateja.
“Ilipofika majira ya saa 4:15 asubuhi jana (juzi), wahudumu wakiwa wanafanya kazi za usafi, ndipo walipomwona PC Donald akiwa kwenye kochi wakidhani amelala lakini walipojaribu kumwamsha hakuamka ndipo walipotoa taarifa polisi.“ameeleza Kamanda Marwa.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma, Dk. Hassan Lumbe, alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, alisema mwili wa askari huyo ulifikishwa hospitalini hapo na watu ambao hawakujitambulisha na ulipokewa na mganga wa zamu.
Dk. Lumbe alifafanua kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kitabibu ilionekana kuwa askari huyo ameshafariki dunia muda mrefu uliopita na kwamba uchunguzi huo ulionyesha hakuwa na mchubuko wowote.
Baadaye walipohojiwa watu waliomleta kwenye Bar hiyo, walidai kuwa alikuwa amekunywa kiasi kikubwa cha pombe.
Comments
Post a Comment