HOFU YATANDA SIMBA KUTOLEWA LIGI YA MABINGWA AFRIKA


SIMBA inatarajiwa kucheza dhidi ya TP Mazembe katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baadaye mwezi ujao, lakini huko mitandaoni kuna taarifa ambazo zinaweza kuwashtua Wanasimba na Watanzania kwa jumla.

Kwa mujibu wa mtandao mmoja wa Afrika Kusini ambao umekuwa ukiandika habari mbalimbali za michezo ya Afrika, kuna hofu kuwa yawezekana Simba ikaondolewa mashindanoni na kisha nafasi hiyo ikaenda kwa AS Vita Club ya DR Congo.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa kuna malalamiko ya Vita juu ya Simba ambao ndiyo waliowatoa katika mechi ya mwisho ya Kundi D na kufanikiwa kusonga mbele, kuwa waliwekewa dawa za kuwamaliza nguvu kwenye vyumba vya michezo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kulikochezwa mchezo huo.

Simba ilifuzu hatua hiyo na kuweka historia baada ya kuifunga Vita mabao 2-1 huku bao la dakika za mwisho likifungwa na Clatous Chama, hivyo kuungana na Al Ahly katika kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa kutoka kundi lao D.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kiongozi mmoja wa soka wa DR Congo, Constant Omari ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Soka la Kimataifa (Fifa), ametoa ripoti juu ya kilichotokea katika mchezo huo wa Simba na Vita.

Katika mchezo huo wachezaji na makocha wa Vita waligoma kutumia vyumba vya kubadilishia nguo uwanjani hapo na badala yake wakavalia kwenye korido huku baadhi yao wakiwa wameziba pua na mdomo kwa vitambaa maalum.

Mbali na hapo, mwandishi mmoja kutoka Ghana ambaye amekuwa akiandika katika mtandao wa Ghana Soccer Net, ameelezea kuwa, Simba walihusika katika kuweka dawa mbaya kwenye vyumba vya wachezaji.

Kupitia ukurasa wake, mwandishi huyo alisema uchunguzi unaendelea huku mabosi wa AS Vita wakiwa makini kuendelea kufuatilia suala hilo. Amesema kuwa Simba wameonyesha kuwa tayari kufanyika kwa uchunguzi wa suala hilo na kudai kuwa madai ya Vita ni ya uongo na wao wapo tayari kwa ajili ya uchunguzi kama utahitajika.

Mwandishi huyo ameandika kuwa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) linaendelea na uchunguzi na kudai kuwa pia kulikuwa na malalamiko ya aina hiyo kwa Al Ahly ya Misri ilipocheza na Simba uwanjani hapo hivi karibuni. Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Simba, Vita na Caf mara baada ya taarifa hii kusambazwa.

Comments

Popular Posts