MO AANDA SILAHA HATARI KUIUA MAZEMBE


BAADA ya ratiba ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwekwa hadharani, uongozi wa Klabu ya Simba ulikutana jana Ijumaa kwa ajili ya kuweka mikakati na mipango yao kuelekea mchezo wao dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Jumatano ya wiki hii Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilichezesha droo kwa ajili ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Simba ilipangwa na TP Mazembe ya DR Congo, Mamelodi Sundowns dhidi ya Al Ahly, Horoya dhidi ya Wydad Casablanca.

Viongozi wa klabu hiyo walikutana kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuhakikisha wanaona Simba inasonga mbele kwenye michuano hiyo kwa kufanya vyema dhidi ya Mazembe.

Simba kwa sasa ipo chini ya mwekezaji wao, Mohammed Dewji ‘Mo’ akishirikiana na Mwenyekiti ya Bodi wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi, Mtendaji Mkuu Crescentius Magori na viongozi wengine.

Katibu wa klabu hiyo, Dk Anold Kashembe, alisema kuwa viongozi wamejipanga kukutana kwa ajili ya kuwajadili Wakongo.

“Ndiyo ratiba imeanikwa wazi tayari ya robo fainali, tumepangwa na TP Mazembe lakini kwetu una umuhimu mkubwa kwa hatua tuliyofikia.

“Na baada ya kikao hicho, ndipo tutajua tunaanzia wapi kwenye maandalizi ingawa timu tayari ilianza maandalizi yake tangu hatua ya awali mpaka hapa ilipofika sasa na mengine yatawekwa hadharani wakati ukifika,” alisema Kashembe.

Ikumbukwe Simba ilifanikiwa kuitoa AS Vita Club katika hatua ya makundi kwenye mchezo wake wa mwisho na kutinga robo fainali.

Comments