YANGA YAPEWA MASHARTI MAZITO KUMNG'OA STRAIKA COASTAL UNION
Wakati Yanga wakiwa katika mipango ya kumsajili mshambuliaji wa Coastal Union, Ayoub Lyanga, meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo ametoa masharti juu ya usajili wake.
Lyanga mwenye mabao 10 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, anatakiwa na Yanga kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongozwa na Heritier Makambo.
Kisongo alisema kama Yanga inataka kumsajili mchezaji huyo, basi ifahamu kuwa kutakuwa na kipengele cha kumuachia kama ikitokea kuna timu nje ya Tanzania itamhitaji hapo baadaye.
“Lyanga ni mchezaji mzuri tena sana ndiyo maana timu nyingi zinamhitaji ikiwemo Yanga na nyingine nje ya Tanzania.
“Mipango yetu ni kuona kijana akicheza soka nje ya Tanzania, lakini kama kuna timu ya ndani itakuja na ofa nzuri zaidi mapema basi mazungumzo yatafanyika kwa ajili ya kujiunga nayo.
“Nimesikia Yanga inamtaka, lakini si hao tu, kuna timu nyingi za ndani na nje zinamtaka pia, yeyote atakayekuja kwa ajili ya kumsajili hasa kwa timu za ndani, zifahamu kwamba kutakuwa na kipengele hicho cha kumuachia ikitokea nafasi nje ya nchi imepatikana,” alisema Kisongo.
Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuitumikia Zanaco ya Zambia, ana uwezo wa kucheza namba 7, 9, 10 na 11.
Comments
Post a Comment