ACHENI KULALAMIKA, UNACHOPATA SASA NI KILE ULICHOPANDA 2018/19



NA SALEH ALLY

USAJILI umekuwa ukipamba moto kwa kila
klabu kwa sasa. Kila upande unataka kujiweka
vizuri kwa ajili ya msimu ujao.


Hili si zoezi geni kutokea katika mchezo wa
soka kwa kuwa kila baada ya msimu kwisha,
taratibu za kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao
Huanza.


Wakati usajili unaendelea, unaona namna
ambacho kinafanyika, wachezaji wengi kutoka
nje wameendelea kuwa gumzo na lazima
wanafaidika sana.


Naweza kusema wachezaji hao wanafaidika
kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watakuwa
wametengeneza majina kwa kiasi chao au
ikiwezekana nchi wanazotokea.


Kama ambavyo ukisikia mchezaji anayetokea
Brazil, Afrika Magharibi au Afrika Kaskazini.
Wachezaji wa ndani wameendelea pia kupata
nafasi lakini idadi yao ni chache sana.


Mfano kama kila timu ya Ligi Kuu Bara itasajili
wachezaji 25, maana yake ligi itakuwa na

wachezaji 500 na kati ya hao, wageni wastani
wao ni wachezaji angalau 40 tu kwa kuwa timu
zenye uwezo wa kusajili wachezaji wa kigeni
hazizidi sita.


Tatu ambazo ni Simba, Yanga na Azam FC
zinaweza kukamilisha idadi ya wachezaji 10
lakini nyingine ni wachezaji wawili, watatu
angalau watano ambazo pia ni chache sana.
Kwa mfano huo, maana yake iko hivi; wachezaji
wengi wa nyumbani au wazalendo ndiyo
wangepaswa kusikika zaidi kwa kuwa idadi ni
Kubwa.


Mfano kwa kipindi hiki, kama ambavyo Simba
imemsajili Kennedy Juma au Yanga Ally Ally
ambao wote ni wawili, basi idadi kubwa
ingekuwa inatokea nyumbani.


Mambo yako tofauti kidogo kwa kuwa nguvu
kubwa inaelekezwa kwa wachezaji wa kigeni.
Klabu zinaangalia wachezaji wa kigeni
kutokana na kuamini ubora wao.


Klabu zinaangalia wachezaji wa kigeni kwa
kuwa kuna rekodi zinazoonyesha wamefanya
vizuri katika sehemu nyingi. Sote tunakubali
Simba ndiyo timu bora zaidi msimu uliopita,
unaona namna wageni walivyokuwa msaada
mkubwa.


Upande wa Yanga, unaona wageni kama
Heritier Makambo, ameondoka kwenda Guinea,
lakini ameacha alama na kufanya Yanga
ipambane kuziba pengo lake kwa kutafuta
mgeni mwingine.


Kama Yanga ingekuwa imeona mshambulizi
mkali zaidi wa nyumbani, huenda ingefanya
hivyo. Binafsi nilifikiri Salim Aiyee angeweza
kuwa kati ya wanaofuatiliwa kwa karibu.
Ukiachana na ninavyoona, katika wazalendo
Aiyee hakutendewa haki. Najiuliza wazalendo
wengine ambao ni wengi, wanaona walifanya
vema na kustahili kuwa gumzo wakati wa
usajili?


Idadi ya gumzo la wageni ambao ni wachezaji,
limefunika kabisa gumzo la wenyeji. Huu ndiyo
wakati wa mavuno, unachopata ni kile
ulichokihangaikia wakati wa kulima.


Jiangalieni na mjiulize, mlilima kwa kiasi gani
na mnastahili kuvuna nini? Nawakumbusha
unapokuwa unapambana basi ujue utafikia
wakati wa mavuno ambao una faida zake.
Maana yake ni hivi, unapokuwa unapambana

wakati wa msimu unaendelea, ujue ubora wa
kazi yako wakati huo ndio utakuwa mafanikio
yako hapo baadaye ikiwa ni pamoja na kupata
ofa ambazo zitaongeza wigo wa kipato chako.


Usije ukawa katikati ya msimu ukadhani timu
unayoitumikia unaisaidia. Unajisaidia wewe na
kutengeneza njia sahihi ya kutimiza ndoto zako.
Kama wakati huu unajiona mnyonge na timu
imemaliza mkataba na wewe, basi tambua
chanzo cha unyonge huo ni wewe mwenyewe.

Comments

Popular Posts