AZAM FC YAMSAJILI MVUYEKURE WA KMC, CHIRWA NA HOZA NAO WASAINI MIKATABA MIPYA


UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, umekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Emmanuel Mvuyekure, kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea KMC.
Mvuyekure anayemudu nafasi zote za ushambuliaji, anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Azam FC kuelekea msimu ujao baada ya ule wa kwanza wa winga idd 'Nado'. Mbali na kusaidia pasi za mwisho za mabao akiwa KMC msimu uliopita, nyota huyo raia wa Burundi alimaliza msimu akiwa na mabao 10.
Nyota huyo aliyewahi kucheza Mbao na KMC, tayari ameshatua nchini leo alfajiri na leo usiku anatarajia kuanza rasmi mazoezi na kikosi hicho kilichoanza maandalizi ya msimu mpya jana jioni.


Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akisaini mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia Azam FC



Kiungo mzawa, Salmin Hoza akisaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Azam FC

Kocha Mkuu mpya wa Azam FC, Etienne Ndayiragije, ndiye aliyependekeza usajili wa nyota huyo, ambapo hadi sasa katika mapendekzo ya usajili wa nyota wapya wanne, amebakisha nafasi mbili, mmoja akiwa wa ndani na mwingine wa nje.
Katika hatua nyingine, mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa, ataendelea kuitumikia timu hiyo baada ya kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja.
Chirwa aliyefunga bao muhimu kwa Azam FC kwenye mechi ya mwisho msimu uliopita katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Lipuli FC ya Iringa, tayari ameanza maandalizi ya msimu mpya na kikosi cha timu hiyo jana.
Naye kiungo Salmin Hoza, ameongeza mkataba wa mpya wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji na mashuti ya mbali, ataendelea kusalia kwenye viunga vya Azam Complex hadi 2021 na tayari ameshaanza maandalizi ya msimu mpya jana.


Comments

Popular Posts